Ukiachana na jinsi ya kuongeza ujazo wa uhifadhi katika simu za Android, hapo nyuma tuliandika kuhusiana na jinsi gani tunaweza tukaongeza ujazo katika simu za iPhone.
Kusoma juu ya kuwezesha hilo katika iPhone soma hapa
Simu zinazotumia program endeshaji ya Android ndizo zinazoongoza kutumiwa duniani kote. Mara nyingi watu wanapata changamoto kwani vifaa hivyo huwa vinajaa mara kwa mara. Mambo yamekua mengi sana siku hizi na yote yanahitaji nafasi katika vifaa vyetu
Tuzifahamu Njia Hizo
1. Futa App Za Zamani Na Zile Ambazo Huzitumii
Kuna uwezekano mkubwa sana kwamba App zetu zinatumia ujazo wa uhifadhi mwingi sana katika vifaa vyetu vya Android. Hapa cha msingi ni kuweza kufuta App hizo zote ambazo ni za zamani na ambazo mtu hazitumii kwa wakati huo. Hii inatokwa mara nyingi, utakuta mtu alishusha mchezo (gemu) na baadae akalichoka lakini akawa hakulifuta. Hilo litakuwa ni moja kati ya mambo yanayojaza ujazo wa uhifadhi
Kufuta App Nende katika – Settings
– Ingia katika Applications au Apps
– Ingia katika App Ambayo unataka kufuta
– Na kisha Uninstall ili kuifuta
2. Futa Mambo Uliyoyashusha (download) Ambayo Hayana Umuhimu Tena
Kama una tabia ya kushusha mambo mengi sana katika mitandao basi hii inakuhusu. Kumbuka sio wote wenye simu za Android kwenye vifaa vyao vina ile sehemu iliyoandikwa Downloads, ya kwako inaweza ikawa imeandikwa My Files au kitu kama hicho. Sehemu hizo ndio zinahifadhi mambo yote tunayoyashusha kama vile nyaraka mbali mbali, picha na kadhalika
Kufuta Vitu Hapo ingia katika – My Files au katika simu zingine ingia katika Downloads
– Ingia katika Downloads
– Chagua faili unalotaka kulifuta kwa kuligusa
– Baada ya hapo bonyeza katika kile kialama cha kufuta
3. Futa Miziki
Hapa kidogo wengine wanaweza wakawa watata,sawa tunapenda miziki kwa kiasi kikubwa sana. Sema ngoja nikuulize swali. Je huwa unasikiliza miziki yote katika simu yako? Namaanisha YOTE? Au ndio kuna mingine huwa unaruka ruka? Kama ukiwa na jibu basi hiyo ambayo huwa unaruka ruka inabidi uifute ili kuongeza ujazo wa uhifadhi katika kifaa chako cha Android
Au ukitaka unaweza ukatumia huduma za muziki wa ku’stream’. Huduma hizi huwa hazily ujazo mwingi wa uhifadhi katika vifaa kama zile njia zetu za kawaida za kuhifadhi nyimbo
4. Futa Video Zenye Ujazo Mkubwa
Ushawahi kuona mtu ana video nyingi katika simu yake kama vile kazi yake ni u’Director’? (haha!). kuna watu wana video nyingi sana katika simu zao. Kwa mfano mtu anaweza akawa na simu imejaa video nyingi sana za vichekesho, kumbuka kuna video nyingi sana za vichekesho na kamwe huwezi ukawa nazo zote. Kama video hizo zikiwa ni za muhimu sana basi huna budi kuzihamishia katika kompyuta na kisha ukafuta katika simu yako
5. Tumia Memori Kadi (MicroSD Card)
Kumbuka sio kila simu zote za Android zina uwezo wa kukubali memori kadi. Zingine zinakuja na ujazo wa ndani tuu. Kama wewe simu yako inaruhusu memori kadi basi huna budi kutafuta moja ambayo itakusaidia kuweka vitu vyako. Memori ziko za ujazo tofauti tofauti kulingana na mafaili yako tuu unayohifadhi.
6. Tumia uhifadhi wa mtandaoni
Kama bado unaona ujazo hautoshi na una mambo mengi sana huna budi kuwa unatumia uhifadhi wa mtandaoni. Ili kuweza kuhifadhi mafaili yako (picha, miziki, video, nyaraka n.k) bofya hapa