NASA imetuma chombo ambacho kitachukua sampuli ya mchanga kwenye mwamba uliopo kwenye sayari ndogo (Asteroid) yenye upana wa mita 500 ijulikanayo kama ‘Bennu’.
Wanasayansi wanatumaini sampuli hiyo itafichua maelezo ya kina juu ya taarifa za sayari zote na hivyo kuboresha uelewa wao kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na vifaa vya angani vinavyotoka kwenye mfumo wa Jua.
Chombo hicho kilichoitwa jina la Osiris-Rex, kiliondoka kuelekea anga za mbali kutoka Florida. Itakichukua miaka saba kabla ya chombo hicho kurejea duniani. Kinatarajia kuisogelea Bennu (Asteroid) mwaka 2018.
Sampuli hiyo itarejeshwa katika pipa litakaloshushwa kwenye jangwa la Utah tarehe 24 Septemba 2023 na ilieleweke kuwa si sampuli itakayokuwa ya kwanza kurejeshwa duniani na chombo cha anga za mbali.
Wajapan walirejesha kiasi kidogo cha vumbi kutoka kwenye sayari ndogo (Asteroid) katika eneo la ‘Itokawa‘ mwaka 2010 lakini Wamarekani wanatumaini kupata sampuli hiyo kwa wingi zaidi; yenye uzito labda wa gramu mamia kadhaa.
Wahandisi wametengeneza kifaa cha kutunza sampuli hizo ambacho kimewekwa kwenye Osiris-Rex katika mkono wa roboti na kwenye eneo la juu la ‘Bennu‘.
TeknoKona itaendelea kufuatili kuhusu hili na kuleta masasisho (updates) kuhusiana na jambo hili.
Vyanzo: BBC, NASA