Kampuni ya Facebook imekuwa imejikita katika utengenezaji wa ndege ndogo zinazotumia umeme wa jua zitakazokuwa na uwezo wa kurusha huduma ya intaneti kwa mamilioni ya watu watakuwa eneo ambalo ndege hizo zitakuwa zinaruka.
Ndege ilifanikiwa kuwa hewani kwa takribani dakika 90, ila ilipata hitilafu na kuanguka wakati ikijaribu kutua. Ndege hizi ndogo zinatumia umeme wa jua kupaa na kurusha huduma ya intaneti kwa eneo la chini – hii italenga sehemu zinazokosa huduma hiyo au huduma hiyo inapatikana kwa shida.
Majaribio ya ndege hiyo iliyopewa jina la Aquila yalifanyika mwezi Juni tarehe 28 mwaka huu.
Ndege hiyo ilifanikiwa kupaa bila shida yeyote, waandisi wa kampuni hiyo walifanikiwa kusoma data mbalimbali zinazohusu majaribio hayo wakati ndege hiyo ikiwa angani – tatizo pekee lilitokea pale tuu ndege ilipokuwa inatua.
Mpango mzima ulikuwa kufanya majaribio hayo kwa muda wa dakika 30 ila baada ya ndege hiyo kuwa angani ulifanyika uamuzi wa kuiweka ndege hiyo angani kwa muda mrefu zaidi.
Tatizo lilitokeaje?
Eneo la majaribio ni eneo la jangwa na kila muda ulivyokuwa unazidi kwenda ndio anga likawa na joto zaidi na upepo mkali. Vitu hivi vilichanganya mfumo wa kompyuta wa kuindesha yenyewe ndege hiyo na hivyo makosa ya kimaesabu yalisababisha ndege hiyo iende kwa kasi zaidi kitu kilichasababisha bawa lake moja kuharibika na hivyo kuiangusha vibaya ndege hiyo wakati inajitahidi kutua.
Nini wamejifunza Facebook?
Wenyewe wamesema lengo lao la kujifunza zaidi limekamilika. Lengo lao kwa ndege hizo ni kuruka na kutumika mara moja tuu. Kikubwa ni kwamba ilifanikiwa kupaa vizuri na kukaa angani na kufanya kazi kama malengo yao yalivyo, wataona vitu vya kuboresha na tutegemee kusikia maendeleo zaidi kwenye mpango wao huu.
Huduma ya intaneti kutoka Facebook inakuja. Suala ni ‘LINI’ – tunategemea kwa kiasi wanachowekeza katika teknolojia hii basi hadi kufikia mwaka 2018 kuna uwezekano mkubwa tukaona wakaanza kutoa huduma hiyo.