Apple ni moja ya makampuni makubwa zaidi Marekani na duniani kote, lakini ukweli ni kwamba kwa zaidi ya asilimia 90 ya utengenezaji wa simu na tabelti zake (iPhones na iPad) huwa unafanyika nchini China zaidi, vingine Taiwan na Korea Kusini na si Marekani.
Mshindi wa Urais wa nchini Marekani, Bwana Donald Trump ameweka suala la makampuni ya nchini humu kuzalisha bidhaa zao ndani ya Marekani kama moja ya sera zake muhimu. Ametishia kuadhibu makampuni ambayo hayatafanya hivyo kwa kodi kubwa zaidi ya iliyopo sasa.
Kwa Apple, kikubwa kwa ofisi zake kuu nchini Marekani ni uongozi wa kiubunifu na mauzo, ila suala zima la utengenezaji hufanywa kupitia muunganisho wa sehemu mbalimbali za bidhaa hizo zinazotengenezwa kupitia makampuni kadhaa nchini China.
Makampuni yanayohusika kukamilisha simu moja ya iPhone ni zaidi ya mia moja na mengi yake yapo nchini China, mengine machache yapo nchini Mongolia, Taiwan na Korea.
Ingawa vyombo kadhaa vya habari vimeripoti ya kwamba tayari Apple wanafikiria kutengeneza simu zao nchini Marekani bado jambo hilo linaonekana ni gumu kutokea. Gharama za uendeshaji Marekani ni kubwa na hili linamaanisha litakula wastani wa faida wanayopata kwa kila simu inayouzika, hili linaweza kuongeza bei za simu hizo.
Changamoto kubwa ni kwamba makampuni kadhaa makubwa yanayohusika katika utengenezaji wa vifaa mbalimbali vinavyotumika katika utengenezaji wa bidhaa za Apple wamesema ni vigumu wao kufikiria kuhamisha viwanda vyao kutoka nchini China kwenda Marekani.
Tovuti ya Digitimes imenukuu makampuni kadhaa ya nchini China yanayohusika na utengenezaji wa simu za iPhone na wengi wao wamesema ni vigumu wao kufanya uamuzi huo.
Kikubwa walichokitaja ni kwamba; gharama za uendeshaji na mishahara ni kubwa mno nchini Marekani.
Kumbuka kusambaza makala na pia kuungana nasi kupitia Facebook, Twitter, Instagram, YouTube, Telegram na Google Plus
Chanzo: Digitimes na mitandao mbalimbali