Hatimaye Kampuni ya Google imefumbua fumbo la herufi O kwa toleo lake jipya la Android 8.0 kwamba herufi hiyo sasa inasimama jina la Oreo.
Tangazo la jina hilo lilitolewa katika jiji la New York muda mfupi baada ya kupatwa kwa jua katika nchi ya Marekani.
Oreo ni aina ya Biskuti tamu za Chokoleti zinazozalishwa na kampuni kongwe ya kimarekani ya Nabisco (National Biscuit Company) yenye makao makuu yake huko East Hanover, New Jersey.
Simu za kwanza kupata toleo la Oreo
Simu za Google Pixel, Nexus 5X na Nexus 6P zitakuwa simu za kwanza kupokea maboresho (Update) za toleo hilo la Android 8.0. Baadae zitafuatiwa na Pixel C na Nexus Player.
Hii ni mara ya pili kwa Google katika historia yake kushirikiana na kampuni ya vitafunio kwenye kuweka jina la toleo la Android. Toleo la kitkat(Version 4.4) lilikuwa na ushirikiano wa kibiashara na kampuni ya Nestle.
Hata hivyo inaelezwa kwamba Google haikuilipa kampuni ya Nestle pesa yoyote kwa kutumia jina la Kitkat. Bali ulikuwa ushirikiano wa kirafiki uliotoa fursa kwa kila upande.