Shirika la Majisafi na Majitaka Dar Es Salaam (DAWASCO) limejiunga na mfumo mpya wa kielektroniki wa malipo serikalini uitwao GePG (Government Electronic Payment Gateway system) kuanzia jana, Mei 2 2018.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameyasema hayo wakati akizungumzia shirika lake kujiunga na huduma ya malipo ya mfumo mpya wa serikalini wa GePG; wateja wa Dawasco wataweza kufanya malipo ya ankara zao kupitia akaunti za kwenye simu yaani M-Pesa, tiGo Pesa na Airtel Money.
Mfumo huo mpya umetajwa utalinufaisha shirika hilo kwa sababu utaondoa ulipaji wa tozo za kamisheni ya asilimia 4 kwa miamala ya shirika hilo ambayo awali ilikuwa ikilipwa kwa wakala wa Maxcom na Selcom.
Kwa utaratibu huo mteja atalipa kiasi kisichopungua asilimia 1 kwa kila muamala atakaoufanya tofauti na awali ambapo malipo hayo ya kamisheni yaligharamiwa na Dawasco.
Kufuatia hatua ya kuacha kuwatumia Maxcom na Selcom, Dawasco itaokoa shilingi 2.4 bilioni kwa mwaka kama sehemu ya makato kupitia wakala hao.
Malipo yatafanyika kwa kila mteja kupewa namba maalum (Control Number) ambayo itakuwa na tarakimu 12 na itatolewa bure kwa wateja wote wa Dawasco.