Google imeleta Google Prompt kurahisisha na kuboresha ulinzi kwa watumiaji wake, huduma hii inafanya kazi kwa kutumia njia ya hatua mbili za uthibitisho kabla ya kumruhusu mtumiaji kufungua akaunti yake.
Hatua mbili za uthibitisho ni moja ya huduma ambazo zinasaidia sana kupunguza uhalifu wa mitandaoni,Google Prompt huleta taarifa katika simu uliyoiiandikisha kukuuliza kama kweli unataka kuingia katika akaunti yako hivyo pamoja na kuingiza nywila yako bado utahitaji kukubali katika simu uliyojiandikisha.
Inafanyeje kazi!?
Tuseme kwamba umeibiwa nywila (password); katika hali ya kawaida aliyeiba nywila huitumia nywila hii kufungua akaunti yako na kutuma barua pepe ama kuandika vitu ambavyo wewe usingeandika, lakini kama utakuwa umetumia Google Prompt basi muharifu wa mtandaoni atakapoingiza nywila katika akaunti yako kwa lengo la kuingia wewe utatumiwa ujumbe (notification) na Google Prompt kukuuliza kama unataka kuingia katika akaunti yako na ukikataa basi muhalifu hataweza kuingia katika akaunti yako.
Inamfaa nani!?
Huduma hii ni nzuri kwa mtu yeyote kwa kuwa katika ulimwengu wa sasa kila mtu anahitaji kujilinda vyema na aina yeyote ya udukuzi, pia makosa ya mtandao yamekuwa mengi zaidi siku za hivi karibuni na tayari madhara makubwa yamekwisha tokea baada ya watumiaji kudukuliwa.
Jinsi ya kuwasha huduma hii katika Google!?
Nenda katika akaunti yako ya Google katika Ukurasa wa MY ACCOUNT ambako utaona Sign-in & Security > Signing in to Google > 2-Step Verification. Fuata maelekezo kisha utakuwa umeiwezesha simu yako, kwa watumiaji wa simu za Android watahitaji kuwa na toleo la karibuni zaidi la Google play services wakati watumiaji wa iPhone wao watahitaji kupakua app ya google search ambayo ndiyo inahusika katika kuleta taarifa za mtu kutaka kuingia katika akaunti yako.