Je unatazama video au kufanya kazi ambayo hutaki watu wachungulie na kujua unafanya nini? Basi kampuni ya HP imekuja na laptop inayokulinda dhidi ya wachunguliaji.
HP (Hewlett-Packard) wamekuja na laptop mbili tofauti ambazo vioo (display) vyake vinauwezo wa kupunguza mwanga kwa hadi asilimia 95 kama mtu anaangalia laptop hizo kutoka upande flani – kushoto au kulia.
Teknolojia hiyo walioipa jina la Sure View inasemekana itasaidia kwa kiasi kikubwa kwa watumiaji wanaopenda usiri wa vitu wanavyofanya kwenye kompyuta (laptop) zao. Kuna laptop mbili zitakazokuja na teknolojia hii, laptop za inchi 14. Na Sure View itaweza kuwezeshwa kwa kubosha F12 katika keyboard.
Tafiti zinaonesha udukuzi wa kuchungulia kwa pembeni au nyuma kuona kompyuta za watu mara nyingi zinafanikisha lengo la mchunguliaji – na pia ni njia rahisi zaidi kuliko udukuzi wa kimtandao.
Vipi je wewe huwa upendezwi na suala la watu kuibia ibia kuchungulia unachofanya kwenye kompyuta yako?
Vyanzo: DigitalTrends na mitandao mbalimbali