WhatsApp haina chanzo cha kuingiza Pesa mpaka sasa #Uchambuzi

0
Sambaza

Upo mjadala ambao umekuwa ukiibuka na kupotea mara kwa mara; mjadala wenyewe ni kuhusu WhatsApp. Je, wanaingizaje pesa kupitia programu yao hiyo? Au hawaingizi pesa yoyote?

Kila mjadala huu unapoanza kunakuwa na pande mbili. Kuna wanaosema WhatsApp wanaingiza fedha nyingi na kuna wanaosema WhatsApp haiingizi pesa yoyote. Leo kupitia tovuti yako ya TeknoKona tutakueleza kama ni kweli WhatsApp wanaingiza pesa au la.

Historia ya WhatsApp (WhatsApp ilipotokea).

Whatsapp ilianzishwa mwaka 2009 na Brian Acton na Jan Koum kama njia mbadala ya huduma za mawasiliano ya meseji. Wawili hao waliwahi kufanya kazi Yahoo lakini walijiondoa na kwenda Amerika ya Kusini na baadae walirudi tena Ulaya na kuanzisha WhatsApp.

waanzilishi wa WhatsApp, Brian Acton (Kushoto) na Jan koum (Kulia)

Wazo la kuanzisha WhatsApp lilikuja hususani pale kampuni ya Apple walipoanzisha App Store kwa simu yake ya iPhone ndipo walipoiona fursa. Waasisi wa WhatsApp walipoianzisha lengo lao la kwanza ilikuwa ni programu ya kutoa taarifa kwa rafiki anayekutafuta kujua nini unachofanya. Yaani unaonesha Status yako kama upo Jimu. Unakumbuka zile Status za ‘At the Gym’, n.k.

Kwa mujibu wa mmoja wa waanzilishi wa WhatsApp Jan Koum anasema watu walianza kutumiana Status hizo kama njia ya kuarifiana hususani kwa watumiaji wa simu za iOS. Baadae programu ya WhatsApp iliongeza kipengele cha kutumiana meseji(Chat Message). Kuanzishwa kwa kipengele hicho watu wengi wakaanza kutumia WhatsApp na ikawa moja ya programu maarufu zaidi duniani.

Umaarufu huo ukaambatana na ada ya utumiaji wa WhatsApp kutozwa. Ada ilikuwa ni Dola 0.99 kwa mwaka. Na hii iliwagusa watumiaji wa nchi chache duniani. Mfano hapa Tanzania ilikuwa ni bure na nchi nyingi duniani ilikuwa hivyo pia.

SOMA PIA:  Watu wawili tu ndio hutaweza kuwa'bloku' facebook!

Wakati huu WhatsApp waliendelea kujenga jina lao kwa kufanya mambo mawili makubwa yaliyowasaidia kujenga jina kubwa duniani. Moja kutokiuka faragha za wateja wao. Yaani kutoingilia kuweka wazi mawasiliano ya watumiaji wake na kutoruhusu matangazo.

mapato ya facebook

Mark Zuckerberg, mmiliki wa Facebook aliyeinunua WhatsApp

Pato la dola moja kwa mwaka

Wakati huo mapato ya Whatsapp yalitegemea malipo ya Dola 1 kwa mtumiaji wake kwa muda wa mwaka mmoja. Malipo haya yalikuwa ni kwa baadhi ya nchi duniani – hasa mataifa yaliyoendelea. Hivyo watumiaji wa nchi zingine hawakuwa wanalipia gharama yoyote kupakua na kutumia Whatsapp.

Kwa mwaka wa kwanza mtumiaji wa WhatsApp aliweza kutumia bure na alilazimika baada ya mwaka mmoja kuanza kulipia kiasi cha dola moja kwa mwaka unaofatia. Inaelezwa mapato ya WhatsApp kwa miezi tisa yaliyotangazwa mwaka Septemba 30, 2014 yalikuwa ni dola 1,289,000. Ni kiwango kidogo kulingana na mwitikio wa watumiaji wake.

Kununuliwa kwa WhatsApp

Mnamo januari 2016 Facebook kupitia mmiliki wake Mark Zuckerberg iliinununa WhatsApp kwa kiasi cha Dola bilioni 19. Ni kiwango kikubwa tofauti na uingizaji wake wa Pesa. Kilichopelekea Facebook kuinunua WhatsApp ni ugumu uliokuwepo wa kupambana na WhatsApp. Tayari watu wengi walishaikubali na kufurahia huduma zao.

Na ilikuwa imeanza kuteka watumiaji wengi wa mitandao kama Facebook na mingine. Hili kibiashara lilianza kutia wasiwasi kwa Facebook na kuanza kupambana ni jambo lisilo kuwa na uhakika zaidi.

SOMA PIA:  Simu ndogo unayoweza 'Kuizungushazungusha'

Kwanini whatsApp waliamua kuifanya app yao kuwa bure kabisa?

Baada ya Facebook kuinunua WhatsApp, miaka miwili baadae yaani Januari 18, 2016 WhatsApp iliondoa ada ya usajili ambayo ilikuwa bado hai kwa baadhi nchi zingine. Iliamua kuifanya kuwa bure kwa watumiaji wake wote duniani.

Wiki chache baadae, uamuzi huo wa kuifanya kuwa bure WhatsApp iliongeza watumiaji kufikia bilioni moja wanaotumia programu hiyo. Inaelezwa kwamba Mark Zuckerberg aliwaambia watu wake waondoke katika kuingiza pesa kwa kiwango kidogo na kutafuta chanzo cha kuingiza mapato ya maana na ya muda mrefu kupitia WhatsApp.

Ni kweli WhatsApp haiingizi kiasi chochote cha fedha?

Hili ni swali linaloulizwa na wengi na limekuwa na majibu yenye kubishaniwa sana. Na dhana nyingi zimekuwa zikitolewa. Katika programu WhatsApp hakuna matangazo yoyote yanayoruhusiwa kuonekana. Njia ya kuruhusu matangazo katika programu ni mojawapo ya chanzo cha mapato kwa wamiliki wa programu.

Kuna sababu kubwa moja na ya msingi ya kufanya hivyo ya kutoruhusu matangazo yoyote katika app yao, Hii imesaidia sana kupata watumiaji wengi ambao hawapendi kero za matangazo yanayojitokeza pindi unapofungua programu.

Kuruhusu matangazo kuna ondoa utulivu kwa mtumiaji wa app yako hivyo kupelekea kutopenda kuitumia hasa pale panapokuwa na programu kama hiyo ambazo haziruhusu matangazo.

Wapata pesa kwa kuuza Data?

Baada ya WhatsApp kununuliwa na Facebook watu wengi waliingia woga kwamba yale yaliyosimamiwa na WhatsApp wenyewe kwa facebook yasingiwezekana tena. Wengine wanasema kuwa wanapata pesa kupitia kuuza data za wateja wao kwa mashirika ya kipelelezi duniani kama CIA, FBI, n.k.

SOMA PIA:  Gemu la FIFA 18: Toleo la bure kabisa lapatikana ndani ya siku 1

Hofu hiyo iliondolewa na Facebook baada ya kutoa tangazo kwa watumiaji wake kwamba hawatakwenda kinyume na maadili kwa kutoa faragha za wateja wao. Mwaka 2016 WhatsApp walianza kutumia mfumo wa meseji wa ‘End to End Encryption’. Hii ina maana hakuna mtu katikati anayeweza kufuatilia mawasiliano yenu.

Mfumo huo unawezesha kabla ujumbe haujatumwa unafungwa (encrypted) na haufunguliwi mpaka ufike kwa mpokeaji (decryption). Hii inamaanisha mfumo huu ni salama zaidi na faragha yake ni kubwa.

Hakuna chanzo rasmi cha pesa

Hadi leo hakuna chanzo cha mapato ya wazi ya WhatsApp. hata hivyo maboresho ambayo yamekuwa yakifanywa na WhatsApp kuna mwanga kwamba uelekeo wao ni wa kuanza kutengeneza pesa kwa muda mrefu.

Hapa WhatsApp bila shaka kitakuwa moja ya chanzo chake cha kuingiza pesa nyingi zaidi kupitia makampuni yatakayohitaji kutambuliwa rasmi kwa akaunti za WhatsApp. Njia nyingine ambayo bado haijawekwa wazi lakini inatarajiwa sana ni ya uwezekano wa whatsApp kuweza kuruhusu miamala pesa kutoka akaunti moja kwenda nyingine.

Njia hizi zipo tayari katika programu kama WeChat na Telegram. WhatsApp kwenye uwanja huo akiingia atapiga pesa nyingi zaidi kwa kuwa na mtaji mkubwa wa watumiaji wengi zaidi duniani.

Wigo wa kutengeneza pesa kwa dunia ya sasa mtaji mkubwa ni kuwa na watu wengi. Tuendelee kusubiri tuone WhatsApp itakapoanza kuingiza pesa kwa njia za wazi zinazoeleweka. Lakini kwa sasa hakuna chanzo kinachofahamika wanachoingiza pesa.

Facebook Comments

ZINAZOHUSIANA

Sambaza
Share.

About Author

Ni mpenzi na mfuatiliaji wa mambo ya Sayansi na Teknolojia.

Comments are closed.

error: Hakimiliki @Teknokona!! Wasiliana nasi kuweza kupata ruhusa ya kutumia mhariri@teknokona.com