Mkurugenzi wa Jamii Forums ashikiliwa na polisi kwa kosa la kampuni hiyo inayoendesha moja ya mtandao unaotembelewa zaidi Tanzania kushindwa kutoa data.
“Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, msingi mkuu wa mtandao wa JamiiForums umekuwa kulinda faragha ya watumiaji wake.
Watumiaji wa mtandao wa JamiiForums wako huru kuweka mijadala, kuanzisha mijadala, kuchangia chochote pasipo kuvunja sheria za nchi au kuhatarisha usalama wa taifa.” – FikraPevu
Mkurugenzi mtendaji Bwana Maxence Melo anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya leo. Tuhuma kuu ikiwa ni ‘kukwamisha upelelezi wa makosa ya mtandao’.
Kampuni ya Jamii Media inayomiliki mtandao huo maarufu tayari inajihusisha katika kesi kadhaa mahakamani zinazodai mabadiliko ya sheria ya makosa ya kimtandao. Ina kesi Mahakama Kuu ya Tanzania (Kesi namba 9 ya mwaka 2016); kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya kwa kuwa vinapelekea kuvunjwa kwa haki za msingi za watanzania watumiao mitandao ili kulinda maslahi ya umma kwa kuzingatia vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Masuala ya usalama wa data za watumiaji wa huduma za kimtandao ni suala nyeti sana katika sheria za mataifa mengi yaliyoendelea ila kwa sheria ya makosa ya kimtandao ya nchini mwetu vyombo vya dora vimepewa nguvu kubwa katika uombaji na utoaji wa data hizo.
Tutaendela kufuatilia habari hii kuwataarifu yatakayojiri.