Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mpaka Desemba 2017 imeonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kufikia watu milioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 45 ya Watanzania wote.
Takwimu imeonesha kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa Intaneti mwaka hadi mwaka.
Takwimu ya mwaka 2012 ya watumiaji wa Intaneti ilikuwa ni milioni 7.52 ambayo ni asilimia 17 wakati mwaka 2013 wakaongezeka kufikia milioni 9.31 sawa na asilimia 21.
Mwaka 2014 watumiaji walifikia milioni 12.17 sawa na asilimia 29, mwaka 2015 watumiaji waliongezeka kufikia milioni 17.62 sawa na asilimia 34 na mwaka 2016 idadi ilifika milioni 19.86 sawa na asilimia 40.
Je neno ‘watumiaji’ ni neno sahihi? Tukumbuke ni kawaida mtu kumiliki vifaa vingi vya intaneti.
Data zinaonesha watumiaji wa mitandao ya kijamii kama Instagram na hata Facebook bado ata milioni 10 hawajafikia kwa Tanzania.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa idadi ya watumiaji wa simu za mkononi imefikia milioni 40 kutoka milioni 27.62 mwaka 2012, huku mtandao wa Vodacom ukiongoza kwa kuwa na watumiaji waliojisajili 12,714,297 wakifuatiwa na Tigo kwa kuwa na watumiaji waliosajiliwa 11,062,852.
Katika aina ya Intaneti inayotumika na watu wengi zaidi ni ile inayohamishika yaani ‘wireless’ ina watumiaji wapatao milioni 19 na milioni 3.4 intaneti isiyohamishika na wale wa wanaotumia wired idadi yao ni 520,698.