Simu za Galaxy Note 7 kutoka Samsung zilikuja na zikapewa sifa nzuri sana. Kipindi zinaingia sokoni zilipata sifa ya kuwa moja ya simu janja za kuvutia zaidi kipindi hicho, ila mambo yakabadilika haraka sana na zikatolewa sokoni.
Simu za Samsung Galaxy Note 7 ziliaanza kupata sifa mbaya, baadhi zilianza kulipuka na kuungua. Hali hii ilitokea pale zikiwa kwenye kuchajiwa na ata baadhi zikiwa zimewekwa tuu sehemu. Samsung walihangaika na kufanya mabadiliko ya betri na kuzirudisha tena sokoni lakini wapi haikusaidia – ilifikia hadi kupigwa marufuku simu hizo kubebwa kwenye ndege na sehemu zingine mbalimbali.
Samsung wakaamua kuzitoa simu hizo sokoni, na kwa kulazimisha walituma updates (masasisho) kuzuia ufanyaji kazi wa simu hizo ziweze kurudishwa na watumiaji.
Na sasa miezi baada ya kuwa na mzigo wa simu nyingi kwenye maghala yao na gharama za kuzifumua fumua na kuweza kuepuka uchafuzi wa mazingira imekuwa kubwa sana.
Sasa Samsung wametoa ripoti wakisema asilimia kubwa ya simu hizo zitachambuliwa na kutolewa vitu muhimu kama vile madini muhimu yanayoweza kutumika tena na pia baadhi ya parts zinazoweza kutumiwa kwenye simu za majaribio katika masuala ya utengenezaji.
Ila pia wamesema kuna baadhi ya simu zitaboreshwa na kuuzwa tena kwa bei nafuu. Wengi wanategemea simu hizo zitauzwa zaidi katika masoko ya nchi zinazoendelea. Ila pia inawezekana wakawa wanawapatia wateja wao kuzitumia kwa muda mfupi pale ambapo watakuwa wamepeleka simu zingine kwa matengenezo ya muda mrefu.
Lini?
Katika taarifa ya uamuzi huo Samsung hawajatangaza rasmi tarehe ya upatikanaji na wala bei ya simu hizo. Ila wengi wanategemea zitaanza kupatikana miezi kadhaa baada ya toleo la Samsung Galaxy Note 8 kuingia sokoni. Samsung hawatakubali toleo jipya litoke katika kipindi ambacho Note 7 inarudishwa sokoni.