Kampuni ya Samsung Group ina mpango wa kuwekeza zaidi wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 161 katika kipindi cha miaka mitatu.
Kiasi hiki cha uwekezaji ni sawa na ongezeko la asilimia 6 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na mpango huo unahusisha matumizi ya mtaji katika nyongeza ya tafiti pamoja na kutengeneza vitu mbalimbali vyenye mvuto zaidi.
Katika uwekezaji huo, dola bilioni 116 zitatumika nchini Korea na kuzalisha ajira 40,000 ikiwa ni mara mbili ya idadi iliyokuwa imepangwa.
Aidha, $22bn katika jumla kuu ya uwekezaji huo zitatumika kwenye teknolojia ya upeo wa kufikirika (Artificial Intelligence), uundwaji simu zenye teknolojia ya 5G, vifaa vya kielektroniki kwa ajili ya magari, na pia kujikita katika biashara ya madawa ya kibaiolojia.
Kama hiyo haitoshi, Samsung Electronics imedhamiria pia kujiimarisha kiteknolojia kwa kuongeza idadi ya watafiti wake hadi kufikia 1,000 kwenye vitu vyao vilivyopo Uingereza, Urusi, Canada, Marekani na Korea Kusini.