Saudi Arabia yaondosha marufuku ya kupiga simu za Skype, WhatsApp na Viber. Imeondosha marufuku ya kupiga simu kwa njia ya mtandao kupitia programu/apps kadhaa zenye kuruhusu kufanya hivyo.
Saudi Arabia ilifungia njia za kupiga simu kwa njia ya sauti na video kwa programu za WhatsApp, Skype, Imo, Viber na zingine zenye kufanana na hizo.
Serikali ya Saudi Arabia ilisema kuanzia Jumatano huduma hizo zitapatikana bila yakizuizi chochote. Aidha katika kuruhusu huko Serikali imesema hatua hiyo itarahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi hususani kupitia njia za kimtandao.
Wakati huo huo serikali hiyo imesema itaendelea kuuangalia kwa karibu utumiaji wa huduma hizo. Kwa serikali nyingi huduma hizi zinaleta changamoto katika masuala ya ufuatiliaji wa mazungumzo ya watumiaji wake.
Kwa kawaida ni vigumu sana vyombo vya serikali kuingilia au kuchunguza mazungumzo yanayoendelea kutokana na teknolojia bora za usalama zinazowekwa katika huduma hizi ukilinganisha na mawasiliano ya simu ya kawaida.
Idadi kubwa ya vijana wa saudi Arabia ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii.