Shirikisho la mpira wa miguu duniani, FIFA limeruhusu rasmi matumizi ya teknolojia ya video yaani Video Assistant Refrees (VAR) kutumika katika mechi za Kombe la Dunia 2018 mwezi Juni huko nchini Urusi.
VAR itasaidia kufanya maamuzi ambayo yametolewa na mwamuzi wa uwanjani lakini hayakuwa sahihi na hii itasaidia kupunguza nafasi ya nchi nyingi kurudi nyumbani mapema kutokana na maamuzi yenye makosa.
Kupitishwa kwa teknolojia ya VAR katika kombe la Dunia la mwaka huu kunaweza kuathiri nchi nyingi kuanza kutumia teknolojia hiyo katika ligi zao. Tayari ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga imeanza kutumia pamoja na ligi kuu ya Uhispania, La Liga imeahidi kutumia msimu ujao wa ligi kuu yao.
Teknolojia ya VAR itatumika pale ambapo mwamuzi wa ndani ya uwanja anapopatwa na utata wa alichokiamua, aidha kwa kutoa penati, kumpa mchezaji kadi asiyehusika, mchezaji kujiangusha, kama mpira umevuka goli, mchezaji ameotea au la pamoja na mambo mengine ambayo yanaweza kuwa na uamuzi wenye utata.
Katika hali kama hizo mwamuzi ataruhusiwa kusimamisha mpira na atakwenda kulipokuwa na VAR ataangalia na kujiridhisha kama ni sahihi alichoamua au si sahihi. Mfano kama alikataa goli na teknoojia ya VAR ikaonesha ni goli sahihi basi atabadili maamuzi na kuhesabika ni goli sahihi.
Matumizi ya teknolojia ya VAR yamekuwa ‘Yakililiwa’ kwa muda mrefu sana hasa mwaka 2010 wakati wa kombe la dunia lilipofanyika Afrika ya Kusini katika mechi baina ya Ujerumani na Uingereza mwamuzi alipokataa goli la halali la Frank Lampard kwa kuona mpira haukuvuka mstari wa goli ilihali ulivuka mstari.