App maarufu ya Telegram imeendelea kupata misukosuko baada ya serikali ya Iran kuipiga marufuku nchini humo na badala yake kuzindua programu tumishi mpya yenye maudhui kama ya Telegram.
Kulingana na ripoti ya Al Jazeera serikali ya Iran inawahimiza wananchi wake kutumia programu tumishi mpya waliyoizindua siku ya Alhamisi iliyopita inayoitwa Soroush ambayo inaelezwa kwamba haina faragha yoyote kwa watumiaji wake.
Telegram inakadiriwa kuwa na watumiaji milioni 40 nchini Iran na iliripotiwa kutumiwa na waandamanaji mwaka 2017 kama sehemu ya kuhimizana na kuhabarishana juu ya maandamano.
Kufungwa kwa Telegram na serikali ya Iran ni kwa madai ya kulinda usalama wa taifa hilo. Programu tumishi ya Telegram imekuwa inatumia mfumo wa end-to-end encryption ambao hufanya watu wanaowasiliana kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno ndio wenye kuona hivyo kuwa ngumu kwa mtu wa tatu kuweza kuona kilichotumwa baina ya watu wawili.
Programu tumishi ya Soroush iliyozinduliwa Alhamisi iliyopita inaonekana kuwa na sifa za kawaida ambapo watu wanaweza kutuma/kupokea ujumbe na kupakua video lakini upo wasiwasi mkubwa kwamba serikali inaweza kuwa inafuatailia yote yanayozungumzwa na kujadiliwa na wananchi.