Imekuwa jambo la kawaida pale mgeni anapoongezwa kwenye kundi wana kikundi kumkaribisha lakini itakuaje mtu akiongezwa kwenye kikundi bila ya mtunza kundi kujua?
Watafiti wamewatahadharisha wamiliki wa WhatsApp kuwa app hiyo si salama sana ingawa kuwa na ulinzi ule wa mawasiliano ya watu ni kati yao tu au kwa lugha ya kigeni ni end-to-end encryption.
Katika taarifa ya wazi waliyoitoa kwa Facebook (wamiliki wa WhatsApp) watafiti hao wameweka wazi kuwa kwa yeyote mwenye mamlaka ya kufikia server za WhatsApp basi ana uwezo wa kumuongeza mtu kwenye kundi bila yule mtunza kundi kumuongeza.
Nani mwenye uwezo wa kufikia server za WhatsApp?
Data za watumiaji wa WhatsApp zinaweza kufikiwa na watu wachache tu; wafanyakazi wa kitengo husika, serikali kwa kupitia ombi rasmi na wadukuzi wenye uwezo wa hali ya juu sana.
Facebook wenyewe wanasema hilo si tatizo kubwa sana kwani bado wana njia mbalimbali za kuhakiki kuwa kundi lina wahusika kadhaa na isitoshe mtu mpya atakapoingia kwenye kundi kila mwana kundi anaona na kuonekana kabisa mtu huyo amewekwa na nani.
Watafiti wamependekeza WhatsApp iundwe upya kukabiliana na udhaifu huo uliobainishwa lakini mkuu wa kitengo cha usalama wa WhatsApp anaamini endapo WhatsApp ikiundwa upya basi ule urahisi ilionao kwenye kutumia utapungua.
Vyanzo: Wired, The Verge