Kama umekuwa unamiliki akaunti ya barua pepe katika mtandao wa Yahoo kwa miaka kadhaa sasa badili nywila (password) yako haraka sana.
Taarifa zinaonesha mwaka 2014 mtandao huo maarufu ulidukuliwa na taarifa za watumiaji takribani nusu bilioni (yaani milioni 500) zilivujishwa.
Wenyewe Yahoo wamekubali kuhusu tukio hilo na wamesema wanawasiwasi mkubwa ya kwamba udukuzi huo ulifanywa na wadukuzi wa kimataifa wanaoungwa mkono na taifa flani.
Data za watumiaji zilizodukuliwa ni pamoja na majina ya watumiaji, barua pepe, namba za simu na maswali ya usalama (security questions). Udukuzi huo ulifanyika mwishoni mwa 2014.
Yahoo ina watumiaji takribani bilioni 1 kila mwezi, katika hao kuna wastani wa watumiaji milioni 225 wa barua pepe kila mwezi.
Yahoo tayari ipo katika uangalizi wa kununuliwa na kampuni kubwa ya Marekani, Verizon. Suala hili lazima litawaumiza kichwa Verizon na linaweza likawafanya wajiulize mara mbilimbili.
Yahoo wenyewe wanadai data hizo zimefungwa kiusalama na wanauhakika itashindikana kuzifungua, ila tayari wamewashauri watumiaji wake wabadilishe nywila(password) zao.
Verizon wamesema wataliangalia suala hili na kuona madhara yake.