fbpx

Kwanini blog nyingi za kitanzania hufa?

Google+ Pinterest LinkedIn Tumblr +
Sambaza

Blog ni jukwaa maarufu sana la kutolea na kupata taarifa na maarifa mbalimbali kwenye mtandao. Hivi leo mambo mengi tunayoyasoma kwenye mtandao yapo kwenye blog mbalimbali.

Hivyo basi blog ni jukwaa linaloweza kutumiwa kueneza habari, maarifa pamoja na kujiingizia kipato.

Kwa kulifahamu hili watanzania wengi wamekuwa wakianzisha blog lakini zinakufa au hazifanikiwi jinsi walivyotarajia. Ni vyema ukafahamu kuwa yapo mambo yanayosababisha blog nyingi za kitanzania kufa; hivyo soma mambo haya 8 hapa chini.

1. Kuanzisha blog kwa lengo kuu la kupata pesa

 blog nyingi za kitanzania hufa

Kwa nini blog nyingi za kitanzania hufa?

Ni lazima utambue kuwa pesa ni matokeo ya kutatua shida ya mtu au kumpa mtu kitu au maarifa yenye manufaa kwake. Wamiliki wengi wa blog wa kitanzania hawana lengo tofauti la kuanzisha blog zaidi ya kulenga kupata pesa. Hii ndiyo sababu mtu anafungua blog leo kesho anaweka matangazo kuwa “tangaza nasi hapa”. Nani atatangaza na wewe wakati una watembeleaji 2 kwa siku? Ni lazima ujue kuwa kupata pesa kwenye blog ni lazima ukubali na uwe tayari kulipa gharama ya kufanya kitu chenye manufaa kwa watu.

2. Ubinafsi

Ubinafsi ni tatizo linaloua mambo mengi mazuri ya watu, yakiwemo blog. Watanzania wengi hawapendi kuwashirikisha watu wengine mawazo yao ili washirikiane kwa pamoja kuyatimiza. Ikiwa wewe una wazo fulani kuhusu blog, kwanini usimshirikishe mtu anayeweza kukusaidia mkatimiza wazo hilo? Vivyo hivyo kwa wanaoshirikishwa wengi hawapendi kufanyia kazi wazo lililoletwa na mtu mwingine. Wengi huliiba au kulinakili au hata pengine kulikwamisha tu.

INAYOHUSIANA  Umiliki wa Intaneti; Sasa wa Kimataifa na si Marekani pekee!

3. Kulenga tu kupata watembeleaji (traffic) wengi

Wasomaji au watembeleaji hawaji tu kwenye blog yako kwa sababu unataka waje. Ni lazima kuwa na kitu au sababu inayowafanya watembelee blog yako. Ni lazima kabla hujawaza kuongeza watembeleaji kwenye blog yako ukaandaa vitu vyenye manufaa makubwa kwao. Kamwe, injini pekuzi kama Google na Bing havitoweza kuonyesha blog yako kwa watu kama haina kitu cha maana. Kutokana na jambo hili wengi hujikuta wakishindwa kupata watembeleaji kama wanavyotaka na kujikuta wakiacha kuendeleza blog zao.

4. Kunakili machapisho kutoka blog nyingine

Huu ni ugonjwa mkubwa unaozikabili blog nyingi za kitanzania hasa zile za habari. Habari ikishaandikwa kwenye blog moja, utaikuta kila mahali iko hivyo hivyo. Ni wazi kuwa injini pekuzi kama Google inafahamu makala iliandikwa wapi kwanza; hivyo huzichukulia blog nyingine zilizonakili kama blog zinazokusanya matakataka (blong scraping). Kwa njia hii blog yako kamwe haitapata daraja zuri kwenye matokeo ya utafutaji wa Google (Ranking in Search Engine Result Pages – SERPs).

Kama unataka kuona matokeo mazuri ni lazima ukubali  kutoa jasho uandike makala zako mwenyewe ambazo zitakupa manufaa makubwa.

5. Kutokuwekeza gharama stahiki

Kama nilivyotangulia kusema, blog ni kazi inayohitaji kuwekeza gharama fulani ili uweze kuona matokeo mazuri. Ni lazima uwekeze fedha na muda ili uweze kufanikiwa katika kazi hii. Gharama ya muda na kujitoa ndiyo inayohitajika zaidi kwenye blog. Utahitaji muda wa kutosha kuandaa makala (post) zenye tija kwa wasomaji wako. Muda huu utahusisha kutafiti, kupanga, kuandika na kuhariri machapisho yako ili yawe bora kwa wasomaji.

INAYOHUSIANA  Jua Kuhusu Shindano La Tigo La Waleta Mabadiliko Wa Kidigitali!

6. Kupuuza maarifa ya usanifu mtandao (web design)

Usanifu mtandao hauwezi kutengwa na blog. Kama unataka kuwa blogger mzuri ni lazima uwe pia unafahamu jinsi ya kutumia programu mbalimbali zitakazokuwezesha kutengeneza blog nzuri ambayo ni rafiki pia kwa wasomaji na vifaa vyao.

Manufaa ya kutengeneza blog nzuri:

  • Blog yako itaonekana ni rasmi na ya kitaalamu.
  • Injini pekuzi zitaifurahia na kuiweka juu zaidi kwa wasomaji wengi.
  • Itakuwa rafiki kwenye vifaa kama simu, tablet na kompyuta

Kama huna maarifa ya kusanifu blog, unaweza ukajifunza kwani ni rahisi. Pia unaweza ukatumia watu na kampuni mbalimbali zinazofanya huduma hiyo kwa bei nafuu.Mwonekano

7. Kukata tamaa na kukosa uvumilivu

Mambo mazuri yana milima na mabonde yake. Hili liko wazi pia kwenye blog; ikiwa unataka kufanikiwa kwenye blog basi ni vyema ukajifunza kutokata tamaa na kuwa mvumilivu. Watanzania wengi wenye blog wanakata tamaa pale wanapoona mambo hayaendi kama walivyopanga, huona kuwa blog hailipi wala haina manufaa na kuachia njiani. Lakini ni muhimu ukatafakari kuhusu tovuti kama Teknokona; je ilianza usiku mmoja? Naamini Ndugu Stephen wa TeknoKona anafahamu milima na mabonde waliyopitia kwa miaka kadhaa hadi kufika hapa ilipo leo. Jambo lolote zuri linahitaji kuvumilia na kufanya kwa moyo.

Blog ya TeknoKona imetimiza miaka 6, ilianzishwa tarehe 26 Septemba mwaka 2011. Soma makala yake ya kwanza hapa -> ‘Karibu Teknokona’

8. Makala duni

Kuna mtu mmoja aliwahi kusema kuwa watanzania wengi ni wavivu na hawapendi kusoma. Labda hili ndiyo sababu hata bloggers wengi wa kitanzania hawako tayari kujifunza jinsi ya kuandika makala nzuri kwa ajili ya wasomaji na injini pekuzi. Ni vyema ukafahamu mambo muhimu ya kuzingatia kwenye kila makala unayoiandika kama vile:

  • Uchaguzi mzuri wa kichwa cha makala
  • Mtindo rafiki wa uandishi kwa wasomaji
  • Matumizi ya picha
  • Uboreshaji wa injini pekuzi – Search Engine Optimization(SEO) n.k.
INAYOHUSIANA  Usajili wa kadi za simu kwa njia ya alama za vidole kuanza Mei Mosi 2019 #Tanzania

Ni wazi kuwa ukizingatia mambo haya utaweza kuandaa makala au machapisho (post) nzuri ambazo zitakubalika pia kwa wasomaji wako.

Hitimisho

Naamini sasa umefahamu kwanini watanzania wengi hawafanikiwi kwenye blog. Ni wazi kuwa blog ni kazi kama kazi zingine, hivyo inahitaji marifa stahiki na kuifanya kwa dhati. Naamini kama una blog au una mpango wa kuanzisha ya kwako hutokwamishwa tena na mambo tajwa hapo juu.

Je wewe una blog? Ina mafanikio kiasi gani? Au unafahamu sababu nyingine inayoua blog za watanzania? Tafadhali tuandikie maoni na maswali yako hapo chini kisha usisahau kuwashirikisha wengine.

Facebook Comments

Sambaza
Share.

About Author

Kornel ni mfuasi mkubwa wa maswala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Ana uzoefu mzuri katika maswala mbalimbali yanayohusu kompyuta na teknolojia. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali kama vile kutengeneza tovuti, kutengeneza programu mbalimbali, usanifu picha na video bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali.

Comments are closed.