Biashara ya utengenezaji ndege za abiria nchini China inaonekana kuanza kuchukua sura mpya baada ya mafanikio ya kufanya majaribio ya ndege ya kwanza kabisa kwa ajili ya abiria. Hii italeta ushindani kwa makampuni makubwa kama vile Boeing na Airbus – ya Marekani na Ulaya.
Wiki iliyopita kwa mara kwanza kabisa China walifanikiwa kufanya majaribio ya ndege hii kubwa inayolenga kuwa mwanzo wa utengenezaji wa ndege za abiria nchini humo.
Kwa kiasi kikubwa mafanikio haya kwa China yatasaidia kushusha gharama kubwa ya ununuaji wa ndege za usafiri mpya kutoka barani Ulaya na nchini Marekani.
Tayari ukuaji wa teknolojia ya utengenezaji magari na mabasi kwa nchini China umesaidia kwa kiasi kikubwa watumiaji wa mataifa mengi duniani kote kuweza kupata eneo mbadala la kununua vyombo hivyo vya usafiri kwa bei nafuu – ukilinganisha na bei kutoka makampuni ya Ulaya.
Ndege hii inatengenezwa na kampuni iendayo kwa jina la Comac na safari ya majaribio hewani ilichukua muda wa lisaa limoja na ndege hiyo ilirudi salama bila tatizo lolote.
Je ni salama?
Kama inavyofahamika vipuri vingi vya ndege ni muhimu viwe vya ubora kweli kweli kwani kosa dogo tuu linaweza sababisha ajali mbaya sana.
Sehemu muhimu za ndege kama vile injini, sehemu kuu ya marubani, na eneo la chini la ndege (belly) vyote vimenunuliwa kutoka makampuni nguli kwenye vipuri vya ndege ya nchini Marekani na Ulaya – kama kampuni ya General Electric na Honeywell.
Ndege hiyo inayotumia ‘code’ ya C919 ina uwezo wa kubeba abiria 158 na utengenezaji wa teknolojia nzima hadi kufikia kuikamilisha ndege hii imechukua miaka kumi.
Hadi sasa hivi tayari kampuni hiyo imepata oda za ndege 570 za jamii ya C919 kutoka kwa wanunuaji 23. Wengi wao wakiwa ni makampuni ya ndege ya nchini China na mengine nje ya nchi.
Ndege hii kushindana na familia ya ndege za Airbus 320 na Boeing 737.