Jumapili ya Julai Mosi ilikuwa chungu kwa wananchi wengi wa Uganda baada ya sheria ya kulipia kodi kwa mitandao ya kijamii kuanza rasmi na kushindwa kutumia mitandao hiyo mpaka walipie kodi iliyopitishwa na serikali.
Mwezi mmoja uliopita bunge la nchi hiyo lilipitisha mswada wa sheria mpya ya kuwataka watumiaji wa mitandao ya kijamii kuanza kulipia kodi. Mitandao ya kijamii ambayo itamlazimu mwananchi kuilipia kodi kabla ya kuitumia ni WhatsApp, Facebook, Twitter, Google Hangouts, Yahoo Messenger, Instagram, YouTube, Skype na mingine.
Malipo hayo ya kodi yatafanyika kupitia kupitia kampuni tatu zinazotoa huduma za mawasiliano za MTN, Bharti Airtel na Africell. Ulipaji wa kodi hii hautahusiana na pesa ya kuperuzi kurasa za mitandao ya kijamii (kifurushi cha intaneti) bali utakuwezesha kupata ruhusa ya kuitumia kwa siku. Hivyo, mtumiaji atalazimika kununua kifurushi cha intaneti au kama anacho ila hajalipia kodi hataweza kutumia mitandao hiyo.
Mitandao hiyo ya kijamii itakuwa imefungwa kutumika kwa nchi nzima ya Uganda isipokuwa kwa yule atakayelipia kodi anafunguliwa na kuweza kuitumia kwa siku husika.
Kuanza kutumika kwa sheria hiyo tayari kumeleta usumbufu kwa wananchi wengi kuanzia jana (Julai 1) na leo hivyo kusababisha malalamiko kutoka kila kona ya nchi hiyo. Aidha, baadhi ya wananchi wameona ni bora kuanza kutumia huduma za VPN ili kuweza kukwepa kodi hiyo ya kila siku.