Hatimae mwanzilishi wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa kashfa ya Cambridge Analytica amevunja ukimya na kudai kwamba wamefanya makosa.
Analytica inatuhumiwa kuingilia data za watumiaji milioni 50 wa mtandao wa Facebook. Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wake wa Facebook Zuckerberg amesema kitendo hicho kimewavunjia uaminifu. Hivyo, kutokana na hali hiyo ameahidi kufanyika mabadiliko kadhaa ili kutoingiliwa na kuibwa kwa taarifa za watumiaji wake.
“Tuna wajibu wa kuzilinda taarifa zenu, na kama tukishindwa kuzilinda hatuna sifa ya kuwahudumia, mimi ndiye niliyeanzisha mtandao huu wa Facebook, mwisho wa siku nina wajibika kwa chochote kinachotokea katika mtandao wetu”, mwisho wa kunukuu.
Ameahidi katika kufuatilia matatizo ya sasa na ya zamani amesema atafanya mambo yafuatayo:-
- kuchunguza mitandao yote ambayo inashirikiana na uga wa Facebook kabla ya kufanyiwa mabadiliko ya mwaka 2014 ya namna ya kuweza kupata taarifa ya watumiaji,
- kufanyia uchunguzi kazi za programu za kimitandao zinazotiliwa shaka na
- kupiga marufuku mwanzilishi wa programu yoyote ambayo inagoma ama haitoi ushirikiano katika uchunguzi pamoja na hatua nyingine ambazo wanaona zitafanya Facebook kuwa mahali salama.