Inaonekana kampuni ya Tecno Mobile imeamua kuingia kwenye soko la dunia kwa miguu yote miwili na sio majaribio.
Hili limeonekana zaidi baada ya kampuni hiyo ya simu kutoka nchini China kuingia mkataba wa kimatangazo na moja ya timu kubwa nchini Uingereza, Manchester City FC.
Kwa miaka mingi Tecno wamekuwa wakitengeza simu na kuuza kwa bara la Afrika tuu, ni mwezi wa tisa tuu kwenye utambulisho wa toleo la Tecno Phantom 6 ndio kampuni hiyo ilitangaza rasmi kuanza kuuza simu zake duniani kote.
Bado ni mapema kujua mafanikio yao ya haraka ila baada ya mwaka au miaka miwili tutaweza kujua nafasi yao katika ushindani mkubwa wa soko ulio tawaliwa na makampuni kama vile Apple, Samsung, Huawei na makampuni mengine mengi yenye miaka mingi katika ushindani wa soko la simu la dunia.
Timu ya Manchester City FC ni moja ya timu inayofanya vizuri katika ligi kuu ya nchini Uingereza na ipo katika mashindano kimataifa ya barani Ulaya, kupitia mkataba huu inaonekana moja kwa moja Tecno watanufaika kuwafikia kwa urahisi mashabiki mbalimbali wa timu hiyo nchini Uingereza na barani Ulaya – na duniani kote.
Soma Pia;
- Tecno watambulisha Phantom 6 na 6 Plus; Na sasa Kupatikana Duniani kote
- Sifa za Tecno Phantom 6
- Sifa za Tecno Phantom 6 Plus